1. Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake mfalme Belshaza maono yalinitokea mimi, naam, mimi Danieli, baada ya hayo yaliyonitokea hapo kwanza.
2. Nami naliona katika maono; ilitukia, nilipoona, nalikuwako huko Shushani ngomeni, katika wilaya ya Elamu; nikaona katika maono, nami nalikuwa karibu na mto Ulai.
3. Ndipo nikainua macho yangu nikaona, na tazama, mbele ya mto alisimama kondoo mume, mwenye pembe mbili; na pembe zile mbili zilikuwa ndefu; lakini moja ilikuwa ndefu kuliko ya pili, na ile iliyokuwa ndefu zaidi ilizuka mwisho.