Dan. 7:14-27 Swahili Union Version (SUV)

14. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.

15. Basi, mimi Danieli, roho yangu ilihuzunika mwilini mwangu, na hayo maono ya kichwa changu yakanifadhaisha.

16. Nikamkaribia mmoja wa hao waliosimama karibu, nikamwuliza maana ya kweli ya hayo yote. Basi akaniambia, akanijulisha tafsiri ya mambo hayo.

17. Wanyama hao wakubwa walio wanne ni wafalme wanne watakaotokea duniani.

18. Lakini watakatifu wake Aliye juu wataupokea ufalme, na kuumiliki huo ufalme milele, naam hata milele na milele.

19. Kisha nalitaka kujua maana ya yule mnyama wa nne, aliyekuwa mbali na wenziwe wote, mwenye kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma, na makucha yake ya shaba; aliyekula, na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake;

20. na habari za zile pembe kumi zilizokuwa kichwani mwake, na ile pembe nyingine iliyozuka, ambayo mbele yake zilianguka pembe tatu; yaani, pembe ile yenye macho, na kanwa lililonena makuu, ambayo kuonekana kwake kulikuwa hodari kuliko wenzake.

21. Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda;

22. hata akaja huyo mzee wa siku, nao watakatifu wake Aliye juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia watakatifu waumiliki ufalme.

23. Akanena hivi, Huyo mnyama wa nne atakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utakula dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande.

24. Na habari za zile pembe kumi, katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi; na mwingine ataondoka baada ya hao; naye atakuwa mbali na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu.

25. Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.

26. Lakini hukumu itawekwa, nao watamwondolea mamlaka yake, kuipoteza na kuiangamiza, hata milele.

27. Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii.

Dan. 7