Dan. 7:13-22 Swahili Union Version (SUV)

13. Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye.

14. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.

15. Basi, mimi Danieli, roho yangu ilihuzunika mwilini mwangu, na hayo maono ya kichwa changu yakanifadhaisha.

16. Nikamkaribia mmoja wa hao waliosimama karibu, nikamwuliza maana ya kweli ya hayo yote. Basi akaniambia, akanijulisha tafsiri ya mambo hayo.

17. Wanyama hao wakubwa walio wanne ni wafalme wanne watakaotokea duniani.

18. Lakini watakatifu wake Aliye juu wataupokea ufalme, na kuumiliki huo ufalme milele, naam hata milele na milele.

19. Kisha nalitaka kujua maana ya yule mnyama wa nne, aliyekuwa mbali na wenziwe wote, mwenye kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma, na makucha yake ya shaba; aliyekula, na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake;

20. na habari za zile pembe kumi zilizokuwa kichwani mwake, na ile pembe nyingine iliyozuka, ambayo mbele yake zilianguka pembe tatu; yaani, pembe ile yenye macho, na kanwa lililonena makuu, ambayo kuonekana kwake kulikuwa hodari kuliko wenzake.

21. Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda;

22. hata akaja huyo mzee wa siku, nao watakatifu wake Aliye juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia watakatifu waumiliki ufalme.

Dan. 7