11. Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.
12. Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika.
13. Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku.
14. Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa.
15. Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na mfalme.
16. Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.
17. Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli.