1. Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote;
2. na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara.
3. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote.
4. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake.
5. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake.