Dan. 5:3-9 Swahili Union Version (SUV)

3. Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwako Yerusalemu; na mfalme na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wakavinywea.

4. Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe.

5. Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule mkono ulioandika.

6. Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana.

7. Mfalme akalia kwa sauti kubwa, akaamuru waletwe wachawi, na Wakaldayo na wanajimu. Mfalme akanena, akawaambia wenye hekima wa Babeli, mtu awaye yote atakayesoma maandiko haya, na kunionyesha tafsiri yake, atavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atakuwa mtu wa tatu katika ufalme.

8. Basi wakaingia wenye hekima wote wa mfalme; lakini hawakuweza kuyasoma yale maandiko, wala kumjulisha mfalme tafsiri yake.

9. Ndipo mfalme Belshaza akahangaika sana, uso wake ukambadilika, na wakuu wake wakaona fadhaa.

Dan. 5