Dan. 4:1-10 Swahili Union Version (SUV)

1. Mfalme Nebukadreza, kwa watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wanaokaa katika dunia yote; Amani iongezeke kwenu.

2. Mimi nimeona vema kutangaza habari za ishara na maajabu, aliyonitendea Mungu aliye juu.

3. Ishara zake ni kubwa kama nini! Na maajabu yake yana uweza kama nini! Ufalme wake ni ufalme wa milele; na mamlaka yake ni ya kizazi hata kizazi.

4. Mimi, Nebukadreza, nalikuwa nikistarehe katika nyumba yangu, nikisitawi katika nyumba yangu ya enzi.

5. Nikaota ndoto iliyonitia hofu; mawazo niliyokuwa nayo kitandani mwangu, na njozi za kichwa changu, zikanifadhaisha.

6. Basi nikatoa amri kwamba wenye hekima wote wa Babeli, waletwe mbele yangu, ili kunijulisha tafsiri ya ndoto ile.

7. Ndipo wakaingia waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu; nikawahadithia ile ndoto; wao wasiweze kunijulisha tafsiri yake.

8. Bali hatimaye Danieli akaingia mbele yangu, ambaye jina lake ni Belteshaza, kwa kufuata jina la mungu wangu; tena ndani yake inakaa roho ya miungu watakatifu; nikamhadithia ile ndoto, nikisema,

9. Ee Belteshaza, mkuu wa waganga, kwa sababu ninajua ya kuwa roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yako, na ya kuwa hapana neno la siri likushindalo, niambie njozi za ndoto yangu niliyoiona, na tafsiri yake.

10. Njozi za kichwa changu kitandani mwangu zilikuwa hivi; naliona, na tazama, palikuwa na mti katikati ya nchi, urefu wake mkubwa sana.

Dan. 4