8. Basi baadhi ya Wakaldayo wakakaribia, wakaleta mashitaka juu ya Wayahudi.
9. Wakajibu, wakamwambia mfalme Nebukadreza, Ee mfalme, uishi milele.
10. Wewe, Ee mfalme, ulitoa amri ya kwamba kila mtu atakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, ni lazima aanguke na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu;
11. na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa katika tanuru ya moto uwakao.
12. Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.
13. Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme.
14. Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha?