1. Nebukadreza, mfalme, alifanya sanamu ya dhahabu, ambayo urefu wake ulikuwa ni dhiraa sitini, na upana wake dhiraa sita; akaisimamisha katika uwanda wa Dura, katika wilaya ya Babeli.
2. Ndipo Nebukadreza akatuma watu kuwakusanya maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, ili wahudhurie wakati wa kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadneza aliyoisimamisha.
3. Ndipo maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, wakakusanyika ili kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha; wakasimama mbele ya ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.
4. Ndipo mpiga mbiu akapiga kelele akisema, Enyi watu wa kabila zote, na taifa, na lugha, mmeamriwa hivi,
5. wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, lazima kuanguka na kuiabudu sanamu ya dhahabu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.
6. Na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa saa iyo hiyo katika tanuru ya moto uwakao.
7. Basi wakati huo, watu wa kabila zote walipoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, watu wote na mataifa na lugha wakaanguka, wakaiabudu ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.
8. Basi baadhi ya Wakaldayo wakakaribia, wakaleta mashitaka juu ya Wayahudi.