31. Wewe, Ee Mfalme, uliona, na tazama, sanamu kubwa sana. Sanamu hii, iliyokuwa kubwa sana, na mwangaza wake mwingi sana, ilisimama mbele yako; na umbo lake lilikuwa lenye kutisha.
32. Na sanamu hii kichwa chake kilikuwa ni cha dhahabu safi; kifua chake na mikono yake ni ya fedha; tumbo lake na viuno vyake ni vya shaba;
33. miguu yake ni ya chuma; na nyayo za miguu yake nusu ya chuma na nusu ya udongo.
34. Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande.
35. Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote.
36. Hii ndiyo ile ndoto, nasi tutaihubiri tafsiri yake mbele ya mfalme.
37. Wewe, Ee mfalme, u mfalme wa wafalme, na Mungu wa mbinguni amekupa ufalme, na uwezo, na nguvu, na utukufu;
38. na kila mahali wakaapo wanadamu, wanyama wa kondeni na ndege wa angani amewatia mkononi mwako, naye amekumilikisha juu ya hao wote; wewe u kichwa kile cha dhahabu.
39. Na baada ya zamani zako utainuka ufalme mwingine mdogo kuliko wewe; na ufalme mwingine wa tatu wa shaba, utakaoitawala dunia yote.
40. Na ufalme wa nne utakuwa na nguvu mfano wa chuma; kwa maana chuma huvunja vitu vyote na kuvishinda; na kama chuma kisetavyo vitu hivi vyote, ndivyo utakavyovunja-vunja na kuseta.
41. Na kama vile ulivyoziona hizo nyayo za miguu na vidole vyake, kuwa nusu udongo wa mfinyanzi, na nusu chuma, ufalme ule utakuwa ufalme uliogawanyika; lakini ndani yake zitakuwako nguvu za chuma, kama vile ulivyoona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope.
42. Na kama vidole vya zile nyayo vilikuwa nusu chuma na nusu udongo, kadhalika ufalme ule utakuwa nusu yake una nguvu, na nusu yake umevunjika.