Dan. 2:1-10 Swahili Union Version (SUV)

1. Hata katika mwaka wa pili wa kumiliki kwake Nebukadreza, Nebukadreza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika, usingizi wake ukamwacha.

2. Ndipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na wasihiri, na Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake. Basi wakaingia, wakasimama mbele ya mfalme.

3. Mfalme akawaambia, Nimeota ndoto, na roho yangu imefadhaika hata niijue tafsiri yake.

4. Ndipo hao Wakaldayo wakamwambia mfalme, kwa lugha ya Kiaramu, Ee Mfalme, uishi milele; tuambie sisi watumishi wako ile ndoto, nasi tutakuonyesha tafsiri yake.

5. Mfalme akajibu, akawaambia Wakaldayo, Neno lenyewe limeniondoka; msiponijulisha ile ndoto na tafsiri yake, mtakatwa vipande vipande, na nyumba zenu zitafanywa jaa.

6. Bali kama mkinionyesha ile ndoto na tafsiri yake, nitawapa zawadi na thawabu na heshima nyingi; basi nionyesheni ile ndoto na tafsiri yake.

7. Wakajibu mara ya pili, wakasema, Mfalme na atuambie sisi watumishi wake ile ndoto, nasi tutamwonyesha tafsiri yake.

8. Mfalme akajibu, akasema, Najua hakika ya kuwa mnataka kupata nafasi, kwa sababu mmeona ya kuwa lile neno lenyewe limeniondoka.

9. Lakini msiponijulisha ile ndoto, iko amri moja tu iwapasayo; maana mmepatana kusema maneno ya uongo, na maneno maovu, mbele yangu, hata zamani zitakapobadilika; basi niambieni ile ndoto, nami nitajua ya kuwa mwaweza kunionyesha tafsiri yake.

10. Wakaldayo wakajibu mbele ya mfalme, wakasema, Hapana mtu duniani awezaye kulionyesha neno hili la mfalme; kwa maana hapana mfalme, wala bwana, wala liwali, aliyetaka neno kama hili kwa mganga, wala kwa mchawi, wala kwa Mkaldayo.

Dan. 2