Dan. 11:2-9 Swahili Union Version (SUV)

2. Nami sasa nitakuonyesha yaliyo kweli. Tazama, watasimama wafalme watatu katika Uajemi; naye mfalme wa nne atakuwa tajiri kuliko hao wote; naye atakapopata nguvu kwa utajiri wake, atawachochea wote juu ya ufalme wa Uyunani.

3. Na mfalme hodari atasimama, atakayetawala kwa mamlaka kubwa, na kutenda apendavyo.

4. Naye atakaposimama, ufalme wake utavunjika, na kugawanyika katika pepo nne za mbinguni; lakini hautakuwa wa uzao wake, wala hautakuwa kama mamlaka yake ambayo alitawala kwayo; kwa maana ufalme wake utang’olewa, hata kwa ajili ya wengine zaidi ya hao.

5. Na mfalme wa kusini atakuwa hodari; na mmoja wa wakuu wake atakuwa hodari kuliko yeye, naye atakuwa na mamlaka; mamlaka yake itakuwa mamlaka kubwa.

6. Na baada ya miaka kadha wa kadha watashirikiana; kwa kuwa binti wa mfalme wa kusini atakuja kwa mfalme wa kaskazini, ili kufanya mapatano naye; lakini hatakuwa na nguvu za mkono wake sikuzote; wala mfalme yule hatasimama, wala mkono wake; lakini yule binti atatolewa, na hao waliomleta, na yeye aliyemzaa, na yeye aliyemtia nguvu, zamani zile.

7. Lakini katika chipukizi la mizizi yake atasimama mmoja mahali pake atakayeliendesha jeshi la askari, naye ataingia katika ngome ya mfalme wa kaskazini, na kuwatenda mambo, na kuwashinda;

8. na miungu yao, pamoja na sanamu zao, na vyombo vyao vizuri vya fedha na dhahabu atavichukua mpaka Misri; kisha atajizuia miaka kadha wa kadha asimwendee mfalme wa kaskazini.

9. Naye huyo ataingia katika ufalme wa mfalme wa kusini, lakini atarudi mpaka nchi yake mwenyewe.

Dan. 11