16. Maana ajaye kupigana naye atatenda kadiri apendavyo, wala hapana mtu atakayesimama mbele yake; naye atasimama katika nchi ya uzuri, na uharibifu utakuwa mkononi mwake.
17. Naye atakaza uso wake ili aje pamoja na nguvu zote za ufalme wake, naye atafanya mapatano naye; naye atatenda kadiri apendavyo; naye atampa binti wa watu ili amharibu; lakini hilo halitasimama wala kumfaa.
18. Baada ya hayo atauelekeza uso wake kwenye visiwa, naye atavipiga visiwa vingi; lakini mkuu mmoja ataikomesha aibu iliyoletwa na yeye; naam, aibu yake hiyo atamrudishia mwenyewe.
19. Ndipo atauelekeza uso wake kwenye ngome za nchi yake mwenyewe; lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena.
20. Ndipo badala yake atasimama mmoja, atakayepitisha mwenye kutoza ushuru kati ya utukufu wa ufalme wake; lakini katika muda wa siku chache ataangamizwa, si kwa hasira, wala si katika vita.
21. Kisha badala yake atasimama mmoja, mtu astahiliye kudharauliwa, ambaye hawakumpa heshima ya ufalme; naye atakuja wakati wa amani, naye ataupata ufalme kwa kujipendekeza.
22. Na wale wenye silaha mfano wa gharika watagharikishwa mbele yake, na kuvunjika, naam, mkuu wa maagano pia.