1. Katika mwaka wa tatu wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, Danieli, ambaye jina lake aliitwa Belteshaza, alifunuliwa neno; na neno lile lilikuwa kweli; maana ni vita vikubwa; naye akalifahamu neno lile, akaelewa na maono hayo.
2. Katika siku zile mimi, Danieli, nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili.
3. Sikula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia.
4. Na siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa kando ya ule mto mkubwa, Hidekeli;
5. naliinua macho yangu, nikatazama, na kumbe, mtu aliyevikwa nguo za kitani, viuno vyake vimefungwa dhahabu safi ya Ufazi;