Ayu. 9:23-35 Swahili Union Version (SUV)

23. Kama hilo pigo likiua ghafula,Atayadhihaki majaribu yake asiye na kosa.

24. Dunia imetiwa mkononi mwa waovu;Yeye hufunika nyuso za waamuzi wake;Kama si yeye, ni nani basi?

25. Basi siku zangu zina mbio kuliko tarishi;Zakimbia, wala hazioni mema.

26. Zimepita kama merikebu ziendazo mbio;Mfano wa tai ayashukiaye mawindo.

27. Nikisema, Mimi nitasahau kuugua kwangu,Nitaacha kununa uso nikachangamke moyo;

28. Mimi huziogopa huzuni zangu zote,Najua kuwa hutanihesabu kuwa sina hatia.

29. Nitahukumiwa kuwa ni mkosa;Ya nini basi nitaabike bure?

30. Ingawaje najiosha kwa maji ya theluji,Na kuitakasa mikono yangu kwa sabuni;

31. Lakini utanitupa shimoni,Nami hata nguo zangu zitanichukia.

32. Kwani yeye si mtu, kama mimi, hata nimjibu,Hata tukaribiane katika hukumu.

33. Hapana mwenye kuamua katikati yetu,Awezaye kutuwekea mkono sote wawili.

34. Na aniondolee fimbo yake,Na utisho wake usinitie hofu;

35. Ndipo hapo ningesema, nisimwogope;Kwani sivyo nilivyo nafsini mwangu.

Ayu. 9