Ayu. 41:23-33 Swahili Union Version (SUV)

23. Manofu ya nyama yake hushikamana;Yanakazana juu yake; hayawezi kuondolewa.

24. Moyo wake una imara kama jiwe;Naam, imara kama jiwe la chini la kusagia.

25. Anapojiinua, mashujaa huogopa;Kwa sababu ya woga wao huvunjwa moyo.

26. Mtu akimpiga kwa upanga, haumwingii;Wala fumo, wala mshale, wala mkuki wenye ncha.

27. Yeye huona chuma kuwa kama nyasi,Na shaba kama mti uliooza.

28. Mshale hauwezi kumkimbiza;Na mawe ya teo kwake hugeuka kuwa kama makapi.

29. Marungu huhesabiwa kama mabua;Naye hucheka mshindo wa mkuki ukitupwa.

30. Pande zake za chini ni kama vigae vikali;Hutandika malazi kama kuweka chombo cha kupuria nafaka juu ya matope.

31. Yeye huchemsha kilindi mfano wa nyungu;Hufanya bahari kuwa kama mafuta.

32. Hufanya mapito yake kung’aa nyuma yakeHata mtu angedhani kilindi kina mvi.

33. Juu ya nchi hapana aliyefanana naye,Aliyeumbwa pasipo oga.

Ayu. 41