9. Mimi ni safi, sina makosa;Sina hatia, wala hapana uovu ndani yangu;
10. Tazama, yuaona sababu za kufarakana nami,Hunihesabu kuwa ni adui yake;
11. Hunitia miguu yangu katika mkatale,Na mapito yangu yote huyapeleleza.
12. Tazama, nitakujibu, katika neno hili huna haki;Kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mwanadamu.
13. Nawe kwani kumnung’unikia,Kwa vile asivyotoa hesabu ya mambo yake yote?
14. Kwa kuwa Mungu hunena mara moja,Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali.
15. Katika ndoto, katika maono ya usiku,Usingizi mzito uwajiliapo watu,Katika usingizi kitandani;
16. Ndipo huyafunua masikio ya watu,Na kuyatia muhuri mafundisho yao,
17. Ili amwondoe mtu katika makusudio yake,Na kumfichia mtu kiburi;
18. Yeye huizuia nafsi yake isiende shimoni,Na uhai wake usiangamie kwa upanga.
19. Yeye hutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake,Na kwa mashindano yaendeleayo daima mifupani mwake;
20. Hata roho yake huchukia chakula,Na nafsi yake huchukia nyama nzuri.
21. Nyama ya mwili wake huliwa, isionekane;Na mifupa yake isiyoonekana yatokea nje.
22. Naam, nafsi yake inakaribia shimoni,Na uhai wake unakaribia waangamizi.
23. Kwamba akiwapo malaika pamoja naye,Mkalimani, mmoja katika elfu,Ili kumwonyesha binadamu hayo yampasayo;
24. Ndipo amwoneapo rehema, na kusema,Mwokoe asishuke shimoni;Mimi nimeuona ukombozi.
25. Nyama ya mwili wake itakuwa laini kuliko ya mtoto;Huzirudia siku za ujana wake;