Ayu. 31:17-31 Swahili Union Version (SUV)

17. Au kama nimekula tonge langu peke yangu,Mayatima wasipate kulila;

18. (La, tangu ujana wangu alikua pamoja nami kama kwa baba;Nami nimekuwa ni kiongozi cha mjane tangu tumbo la mamangu);

19. Ikiwa nimemwona mtu kuangamia kwa kukosa nguo,Au wahitaji kukosa mavazi;

20. Ikiwa viuno vyake havikunibarikia,Au kama hakupata moto kwa manyoya ya kondoo zangu;

21. Ikiwa nimewainulia mayatima mkono,Nilipoona msaada wangu langoni;

22. Basi bega langu na lianguke kutoka mahali pake,Na mkono wangu uvunjike mfupani mwake.

23. Kwani msiba utokao kwa Mungu ulikuwa na kitisho kwangu,Na kwa sababu ya ukuu wake sikuweza kufanya neno.

24. Ikiwa nimeifanya dhahabu kuwa tumaini langu,Na kuiambia dhahabu safi, Wewe u tegemeo langu;

25. Kama nilifurahi kwa kuwa mali yangu yalikuwa mengi,Na kwa sababu mkono wangu umepata vitu vingi;

26. Kama nililitazama jua lilipoangaza,Au mwezi ukiendelea katika kung’aa;

27. Na moyo wangu umeshawishwa kwa siri,Na midomo yangu imeubusu mkono wangu;

28. Hilo nalo lingekuwa uovu wa kuadhibiwa na waamuzi;Kwani ningemwambia uongo Mungu aliye juu.

29. Kama nilifurahi kwa kuangamia kwake huyo aliyenichukia,Au kujitukuza alipopatikana na maovu;

30. (Naam, sikukiacha kinywa changu kufanya dhambiKwa kuutaka uhai wake kwa kuapiza);

31. Kama watu wa hemani mwangu hawakunena,Ni nani awezaye kumpata mtu asiyeshibishwa na yeye kwa nyama?

Ayu. 31