Ayu. 3:15-26 Swahili Union Version (SUV)

15. Au pamoja na wakuu wenye dhahabu,Waliozijaza fedha nyumba zao;

16. Au, kama kuzikwa mimba iliyoharibika, nisingekuwako;Kama wachanga wasiouona mwanga kabisa.

17. Huko waovu huacha kusumbua;Huko nako hao waliochoka wapumzika

18. Huko wafungwa waona raha pamoja;Hawaisikii sauti yake msimamizi.

19. Wakuu na wadogo wako huko;Mtumishi yu huru kwa bwana wake.

20. Mbona yeye aliye mashakani kupewa mwanga,Na hao wenye uchungu rohoni kupewa uhai;

21. Ambao wangojea mauti, lakini hawayapati;Na kuyachimbulia zaidi ya kutafuta hazina iliyostirika;

22. Ambao wafurahi mno,Na kushangilia watakapoliona kaburi?

23. Kwa nini mtu aliyezibiwa njia kupewa mwanga,Ambaye Mungu amemzingira kwa ukingo?

24. Kwani kuugua kwangu kwaja kana kwamba ni chakula,Na kunguruma kwangu kumemiminika kama maji.

25. Maana jambo hilo nichalo hunipata,Nalo linitialo hofu hunijilia.

26. Mimi sioni raha, wala situlii, wala kupumzika;Lakini huja taabu.

Ayu. 3