Ayu. 3:1-12 Swahili Union Version (SUV)

1. Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake.

2. Ayubu akajibu, na kusema;

3. Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi,Na ule usiku uliosema,Mtoto mume ametungishwa mimba.

4. Siku hiyo na iwe giza;Mungu asiiangalie toka juu,Wala mwanga usiiangazie.

5. Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake;Wingu na likae juu yake;Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe.

6. Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu;Usihesabiwe katika siku za mwaka;Wala kutiwa katika hesabu ya miezi.

7. Tazama, usiku huo na uwe tasa;Wala isiwe ndani yake sauti ya shangwe.

8. Na waulaani hao waulaanio mchana,Hao walio tayari kumwamsha huyo lewiathani.

9. Nyota za mapambazuko yake na ziwe giza;Na utafute mwanga lakini usiupate;Wala usiyaone makope ya asubuhi;

10. Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu.Wala kunifichia taabu machoni.

11. Mbona si kufa mimi tokea mimbani?Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni?

12. Mbona hayo magoti kunipokea?Au hayo maziwa, hata nikanyonya?

Ayu. 3