Ayu. 21:13-29 Swahili Union Version (SUV)

13. Siku zao hutumia katika kufanikiwa,Kisha hushuka kuzimuni ghafula.

14. Walakini walimwambia Mungu. Tuondokee;Kwani hatutaki kuzijua njia zako.

15. Huyo Mwenyezi ni nani, hata tumtumikie?Nasi tutafaidiwa nini tukimwomba?

16. Tazama, kufanikiwa kwao hakumo mkononi mwao;Mashauri ya waovu na yawe mbali nami.

17. Je! Ni mara ngapi taa yao waovu huzimishwa?Na msiba wao kuwajilia?Na Mungu kuwagawanyia uchungu kwa hasira yake?

18. Ili wawe kama mabua makavu mbele ya upepo,Kama makapi yaliyochukuliwa na dhoruba?

19. Mwasema, Mungu huwawekea watoto wa mtu huo uovu wake.Na amlipe mwenyewe, ili apate kuujua.

20. Macho yake mwenyewe na yaone uharibifu wake,Akanywe ghadhabu zake Mwenyezi.

21. Kwani ana furaha gani katika mbari yake baada yake,Hesabu ya miezi yake itakapokwisha katwa katikati?

22. Je! Mtu awaye yote atamfundisha Mungu maarifa?Naye ndiye awahukumuye walioko juu.

23. Mmoja hufa katika nguvu zake kamili,Mwenye kukaa salama na kustarehe;

24. Vyombo vyake vimejaa maziwa,Na mafuta ya mifupani mwake ni laini.

25. Mwingine hufa katika uchungu wa roho,Asionje mema kamwe.

26. Wao hulala mavumbini sawasawa,Mabuu huwafunika.

27. Tazama, nayajua mawazo yenu,Na mashauri mnayoazimia kwa uovu juu yangu.

28. Kwa kuwa mwasema, Nyumba ya huyo mkuu i wapi?Na hema waliyoikaa hao waovu i wapi?

29. Je! Hamkuwauliza wapitao njiani?Na maonyo yao hamyajui?

Ayu. 21