1. Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
2. Je! Mtanichukiza nafsi yangu hata lini,Na kunivunja-vunja kwa maneno?
3. Mara kumi hizi mmenishutumu;Hamwoni haya kunifanyia mambo magumu.
4. Ingawaje nimekosa,Kosa langu hukaa kwangu mwenyewe.
5. Kwamba mtajitukuza juu yangu,Na kunena juu yangu shutumu langu;
6. Jueni basi kuwa Mungu amenipotosha,Na kunizingira kwa wavu wake.
7. Tazama, nalia, Udhalimu, lakini sisikiwi;Naulilia msaada, wala hapana hukumu.
8. Yeye ameiziba njia yangu nisipate kupita,Na kutia giza katika mapito yangu.
9. Amenivua utukufu wangu,Na kuiondoa taji kichwani mwangu.
10. Amenibomoa pande zote, nami nimetoweka;Na tumaini langu ameling’oa kama mti.