Ayu. 15:22-35 Swahili Union Version (SUV)

22. Yeye hasadiki kwamba atarudi kutoka gizani,Naye hungojewa na upanga;

23. Hutanga-tanga ili apate chakula, akisema, Ki wapi?Ajua kwamba siku ya giza i tayari karibu yake;

24. Mateso na dhiki humtia hofu;Humshinda kama vile mfalme aliye tayari kwa vita;

25. Kwa kuwa amenyosha mkono wake juu ya Mungu,Na kuendelea kwa kiburi kinyume cha Mwenyezi;

26. Humshambulia na shingo ngumu,Kwa mafundo makubwa ya ngao zake;

27. Kwa kuwa amefunika uso wake na kunona kwake,Na kuwandisha mafuta kiunoni mwake;Naye amekaa katika miji iliyo ukiwa,

28. Katika nyumba ambazo hapana mtu azikaaye,Zilizokuwa tayari kuwa magofu.

29. Hatakuwa tajiri, wala mali zake hazitadumu,Wala maongeo yao hayatainama nchi.

30. Hataondoka gizani;Ndimi za moto zitayakausha matawi yake,Naye ataondoka kwa pumzi za kinywa chake.

31. Asiutumainie ubatili, na kujidanganya;Kwa kuwa huo ubatili ndio utakaokuwa ujira wake.

32. Jambo hili litatendeka kabla ya wakati wake,Na tawi lake halitasitawi.

33. Atayapukutisha mapooza yake kama mzabibu,Na kuyatupa maua yake kama mzeituni.

34. Kwa kuwa jamii ya hao wasiomcha Mungu watakuwa tasa,Na moto utateketeza mahema yenye rushwa.

35. Wao hutunga mimba ya madhara, na kuzaa uovu,Nalo tumbo lao hutengeza udanganyifu.

Ayu. 15