Ayu. 14:10-22 Swahili Union Version (SUV)

10. Lakini mwanadamu hufa, huifariki dunia;Naam, mwanadamu hutoa roho, naye yupo wapi?

11. Kama vile maji kupwa katika bahari,Na mto kupunguka na kukatika;

12. Ni vivyo mwanadamu hulala chini, asiinuke;Hata wakati wa mbingu kutokuwako tena, hawataamka,Wala kuamshwa usingizini.

13. Laiti ungenificha kuzimuni,Ukanilinda kwa siri, hata ghadhabu zako zitakapopita,Na kuniandikia muda ulioamriwa, na kunikumbuka!

14. Mtu akifa, je! Atakuwa hai tena?Mimi ningengoja siku zote za vita vyangu,Hata kufunguliwa kwangu kunifikilie.

15. Wewe ungeita, nami ningekujibu;Ungekuwa na tamaa ya kazi ya mikono yako.

16. Lakini sasa wazihesabu hatua zangu;Je! Huchungulii dhambi yangu?

17. Kosa langu limetiwa muhuri mfukoni,Nawe waufunga uovu wangu.

18. Lakini, tazama, mlima ukianguka hutoweka,Nalo jabali huondolewa mahali pake;

19. Maji mengi huyapunguza mawe;Mafuriko yake huuchukua mchanga wa nchi;Nawe matumaini ya wanadamu wayaangamiza.

20. Wewe wamshinda nguvu sikuzote, naye hupita aende zakeWabadili sura zake, na kumpeleka aondoke.

21. Wanawe hufikilia heshima, wala yeye hajui;Kisha wao huaibishwa, lakini yeye hana habari zao.

22. Lakini mwili ulio juu yake una maumivu,Na nafsi yake ndani huomboleza.

Ayu. 14