Ayu. 11:8-18 Swahili Union Version (SUV)

8. Ni juu mno kama mbingu; waweza kufanya nini wewe?Ni wenye kina kuliko kuzimuni; waweza kujua nini wewe?

9. Cheo chake ni kirefu kuliko dunia,Ni kipana zaidi ya bahari.

10. Yeye akipita, na kufunga watu,Na kuwaita hukumuni, ni nani basi awezaye kumzuia?

11. Kwani yeye awajua watu baradhuli;Huona na uovu pia, hata asipoufikiri.

12. Lakini mpumbavu aweza kupata ufahamu,Ingawa mwanadamu huzaliwa kama mtoto wa punda-mwitu.

13. Wewe ukiuweka moyo wako kwa uelekevu,Na kumnyoshea mikono yako;

14. Ikiwa una uovu mkononi mwako, uweke mbali nawe,Wala usikubali upuzi kukaa hemani mwako;

15. Hakika ndipo utakapopata kuinua uso pasipo ila;Naam, utathibitika, wala hutakuwa na hofu;

16. Kwa kuwa utasahau mashaka yako;Utayakumbuka kama maji yaliyokwisha pita;

17. Na maisha yako yatakuwa meupe kuliko adhuhuri;Lijapokuwa ni giza, litakuwa kama alfajiri.

18. Nawe utakuwa salama, kwa sababu kuna matumaini;Naam, utatafuta-tafuta kando yako, na kupumzika katika salama.

Ayu. 11