Amu. 9:34-50 Swahili Union Version (SUV)

34. Basi Abimeleki akainuka na watu wote waliokuwa pamoja naye, usiku nao wakauvizia Shekemu kwa vikosi vinne.

35. Huyo Gaali mwana wa Ebedi akatoka nje, akasimama penye maingilio ya lango la mji; naye Abimeleki na hao watu waliokuwa pamoja naye wakainuka kutoka mahali pale walipokuwa wanavizia.

36. Basi Gaali alipowaona hao watu, akamwambia Zebuli, Tazama, watu washuka kutoka katika vilele vya milima. Zebuli akamwambia, Ni kivuli cha milima unachokiona kama ndio watu.

37. Kisha Gaali akasema mara ya pili, akanena, Angalia, watu washuka katikati ya nchi, na kikosi kimoja kinakuja kwa njia ya mwaloni wa Meonenimu.

38. Ndipo Zebuli akamwambia, Je! Kinywa chako sasa ki wapi, hata ukasema Huyo Abimeleki ni nani, hata inatupasa kumtumikia yeye? Je! Hawa sio watu hao uliowadharau wewe? Haya, toka nje sasa, tafadhali, upigane nao.

39. Basi Gaali akatoka nje mbele ya watu wa Shekemu, akapigana na Abimeleki.

40. Lakini Abimeleki akamkimbiza, naye akakimbia mbele yake, wengi wakaanguka waliojeruhiwa hata kufikilia maingilio ya hilo lango.

41. Abimeleki akakaa Aruma; naye Zebuli akawatoa Gaali na ndugu zake, wasikae katika Shekemu.

42. Ikawa siku ya pili yake, watu wakatoka waende mashambani; naye Abimeleki aliambiwa.

43. Naye akawatwaa watu wake, na kuwagawanya wawe vikosi vitatu, nao wakavizia mashambani; naye akaangalia, na tazama, watu walikuwa watoka humo mjini; basi akainuka na kupigana nao, akawapiga.

44. Abimeleki, na vile vikosi vilivyokuwa pamoja naye, wakafuliza kwenda mbele, wakasimama penye maingilio ya lango la mji, na vile vikosi viwili vikawarukia hao wote waliokuwa mashambani, na kuwapiga.

45. Abimeleki akapigana na huo mji mchana kutwa; akautwaa mji, akawaua watu waliokuwamo ndani yake; kisha akaupomosha mji, na kuutia chumvi.

46. Kisha watu wote waliokaa katika ile buruji ya Shekemu waliposikia habari hiyo wakaingia ndani ya ngome ya nyumba ya El-berithi.

47. Abimeleki aliambiwa ya kuwa watu hao wote wa buruji ya Shekemu wamekutana pamoja.

48. Basi Abimeleki akakwea kwenda kilima cha Salmoni, yeye na wote waliokuwa pamoja naye; naye Abimeleki akashika shoka mkononi mwake, akakata tawi moja katika miti, akalishika na kujitweka fuzini mwake; akawaambia hao watu waliokuwa pamoja naye, Haya, mliyoniona mimi kufanya, fanyeni upesi vivyo, kama nilivyofanya mimi.

49. Basi watu hao wote vivyo wakakata kila mtu tawi lake, wakamwandama Abimeleki, wakayaweka hayo matawi pale ngomeni, na kuiteketeza moto hiyo ngome juu yao; basi hivyo watu wote wa hiyo buruji ya Shekemu wakafa, walipata kama watu elfu, waume kwa wake.

50. Ndipo Abimeleki alipokwenda Thebesi, akapanga kinyume cha Thebesi na kuutwaa.

Amu. 9