19. basi ikiwa mmemtendea kwa uaminifu na uelekevu Yerubaali na nyumba yake hivi leo, basi furahini ninyi katika huyo Abimeleki, yeye naye na afurahi kwenu ninyi;
20. lakini kwamba sivyo hivyo, basi, moto na utoke katika Abimeleki na kuwateketeza watu wa Shekemu, na jamaa ya Milo; kisha moto na utoke katika hao watu wa Shekemu, na katika jamaa ya Milo, na kumteketeza Abimeleki.
21. Kisha Yothamu akaenda zake na kukimbia, akaenda Beeri, na kukaa kuko, kwa kumwogopa Abimeleki nduguye.
22. Basi Abimeleki alitawala juu ya Israeli muda wa miaka mitatu.
23. Kisha Mungu akapeleka roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu; nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa udanganyifu;
24. ili kwamba huo udhalimu waliotendewa hao wana sabini wa Yerubaali uje, tena kwamba damu yao iandikwe juu ya Abimeleki ndugu yao, aliyewaua, na juu ya watu wa Shekemu, waliomtia nguvu mikono yake ili awaue hao nduguze.
25. Basi watu wa Shekemu wakaweka watu kumvizia juu ya vilele vya milima, ambao waliwanyang’anya vitu vyao watu wote waliopita njia hiyo karibu nao; naye Abimeleki aliambiwa.
26. Kisha Gaali, mwana wa Ebedi, akaenda pamoja na nduguze, wakavuka na kufika Shekemu; na watu wa Shekemu wakamtumaini yeye.
27. Nao wakatoka kwenda mashambani, wakavuna mashamba yao ya mizabibu, na kuzishindika hizo zabibu, na kufanya sikukuu, kisha wakaingia nyumbani mwa mungu wao, wakala na kunywa na kumlaani huyo Abimeleki.
28. Naye Gaali mwana wa Ebedi akasema, Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tukamtumikie yeye? Yeye, je! Si mwana wa Yerubaali? Na Zebuli siye akida wake? Haya, ninyi watumikieni hao watu wa Hamori, babaye Shekemu; Lakini sisi je! Tumtumikie kwa sababu gani?
29. Laiti watu hawa wangekuwa chini ya mkono wangu! Hapo basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Kisha akamwambia Abimeleki, Haya, ongeza askari zako, utoke nje.
30. Basi hapo Zebuli, aliyekuwa liwali wa mji, alipoyasikia hayo maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, hasira zake zikamwaka.
31. Naye akatuma wajumbe waende kwa Abimeleki kwa siri, akasema, Tazama, Gaali, mwana wa Ebedi, na ndugu zake wamekuja Shekemu; na tazama waufitinisha mji huu kinyume chako.
32. Basi sasa, inuka wewe, usiku, wewe na watu walio pamoja nawe, mvizie mashambani;
33. kisha itakuwa, asubuhi, mara litakapokucha jua, wewe utaamka asubuhi na mapema, na kuushambulia mji huo; tena, angalia, hapo yeye na wale watu walio pamoja naye watakapokutokea nje kupigana nawe, ndipo utapata kuwatenda kama utakavyopata nafasi.