9. Kisha wana wa Israeli walipomlingana BWANA, BWANA akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu.
10. Roho ya BWANA ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye BWANA akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu.
11. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini. Kisha Othnieli, mwana wa Kenazi, akafa.
12. Basi wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu tena mbele za BWANA; naye BWANA akamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu juu ya Israeli, kwa sababu walikuwa wameyafanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA.
13. Huyo Egloni akakutanisha kwake wana wa Amoni na Amaleki; akaenda na kuwapiga Israeli, nao wakauchukua huo mji wa mitende.
14. Wana wa Israeli walimtumikia Egloni mfalme wa Moabu muda wa miaka kumi na minane.
15. Lakini wana wa Israeli walipomlilia BWANA, BWANA akawainulia mwokozi, Ehudi, mwana wa Gera, Mbenyamini, mtu aliyekuwa mwenye shoto; nao wana wa Israeli walimpelekea Egloni mfalme wa Moabu tunu mkononi mwa huyo Ehudi.
16. Ehudi alijifanyia upanga uliokuwa na makali kuwili, urefu wake ulipata dhiraa moja; akaufunga huo upanga ndani ya nguo yake katika paja lake la mkono wa kuume.
17. Kisha akamsongezea Egloni, mfalme wa Moabu, hiyo tunu; basi Egloni alikuwa ni mtu aliyewanda sana.
18. Naye hapo alipokuwa amekwisha kuisongeza hiyo tunu, akawapa ruhusa watu hao walioichukua tunu, wakaenda zao.
19. Lakini yeye mwenyewe akageuka kutoka huko kwenye sanamu zilizokuwa karibu na Gilgali, akasema, Mimi nina ujumbe wa siri kwako wewe, Ee mfalme. Naye akasema, Nyamazeni kimya. Watu wote waliokuwa wanasimama karibu naye wakatoka na kumwacha.
20. Basi Ehudi akamwendea; naye alikuwa anaketi peke yake katika chumba chake cha baridi. Ehudi akasema, Mimi nina ujumbe utokao kwa Mungu kwako wewe. Basi akainuka katika kiti chake.
21. Ehudi akaunyosha mkono wake wa kushoto, akaushika huo upanga kuutoa hapo katika paja lake la kuume, akamtia tumboni mwake;
22. hicho kipini nacho kikaingia ndani pamoja na huo upanga wenyewe; nayo mafuta yakashikamana tena juu ya upanga, kwani hakuutoa tena upanga tumboni; nao ukatokea kwa nyuma.
23. Ndipo Ehudi akatoka nje barazani, akamfungia milango ya hicho chumba na kuifunga kwa ufunguo.