Amu. 3:1-14 Swahili Union Version (SUV)

1. Basi haya ndiyo mataifa ambao BWANA aliwaacha, ili awajaribu Israeli kwa hao, yaani, awajaribu hao wote ambao hawakuvijua vita vyote vya Kanaani;

2. ili kwamba vizazi vya wana wa Israeli wapate kujua ili kuwafundisha vita, hasa wao ambao hawakujua vita kabla ya wakati ule;

3. aliwaacha wakuu watano wa Wafilisti, na Wakanaani wote, na Wasidoni, na Wahivi waliokaa katika kilima cha Lebanoni, toka mlima wa Baal-hermoni mpaka kuingia Hamathi.

4. Naye aliwaacha ili awajaribu Israeli kwa hao, apate kujua kwamba watasikiliza amri za BWANA, alizowaamuru baba zao, kwa mkono wa Musa.

5. Basi wana wa Israeli wakaketi kati ya Wakanaani; hao Wahiti, na hao Waamori, na hao Waperizi, na hao Wahivi na hao Wayebusi;

6. wakawaoa binti zao, na binti zao wenyewe wakawaoza wana wao waume, na kuitumikia miungu yao.

7. Wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakamsahau BWANA, Mungu wao, nao wakawatumikia Mabaali na Maashtorethi.

8. Kwa hiyo hasira za BWANA ziliwaka juu ya Israeli, naye akawauza na kuwatia mikononi mwa Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia; na wana wa Israeli wakamtumikia huyo Kushan-rishathaimu muda wa miaka minane.

9. Kisha wana wa Israeli walipomlingana BWANA, BWANA akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu.

10. Roho ya BWANA ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye BWANA akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu.

11. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini. Kisha Othnieli, mwana wa Kenazi, akafa.

12. Basi wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu tena mbele za BWANA; naye BWANA akamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu juu ya Israeli, kwa sababu walikuwa wameyafanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA.

13. Huyo Egloni akakutanisha kwake wana wa Amoni na Amaleki; akaenda na kuwapiga Israeli, nao wakauchukua huo mji wa mitende.

14. Wana wa Israeli walimtumikia Egloni mfalme wa Moabu muda wa miaka kumi na minane.

Amu. 3