1. Basi watu wa Israeli walikuwa wameapa huko katika Mispa, wakisema, Hapana mtu awaye yote kwetu sisi atakayemwoza binti yake kumpa Benyamini.
2. Basi hao watu wakafikilia Betheli, wakaketi kuko mbele ya Mungu hata jioni, nao wakainua sauti zao na kulia sana.
3. Wakasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, kwani jambo hili kuwa katika Israeli, ya kwamba hivi leo ni kabila moja limepunguka katika Israeli?
4. Kisha ikawa siku ya pili yake, hao watu wakaamka asubuhi na mapema, wakajenga madhabahu huko, wakasongeza sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.
5. Wana wa Israeli wakasema, Katika hizi kabila zote za Israeli ni ipi isiyofika katika mkutano kumkaribia BWANA? Kwa maana walikuwa wameweka kiapo kikuu katika habari za huyo asiyefika kumkaribia BWANA huko Mispa, huku wakisema, Hakika yake atauawa huyo.