Amu. 20:1-8 Swahili Union Version (SUV)

1. Ndipo wana wa Israeli walipotoka; na mkutano ukakutanika kama mtu mmoja, kutoka Dani hata Beer-sheba, pamoja na nchi ya Gileadi wakamkutanikia BWANA huko Mispa.

2. Hao wakuu wa watu, maana wakuu wa kabila zote za Israeli, wakajihudhurisha katika huo mkutano wa watu wa Mungu, watu waume mia nne elfu waendao kwa miguu, wenye kutumia upanga.

3. Basi wana wa Benyamini walipata habari ya kuwa wana wa Israeli wamekwea kwenda Mispa. Wana wa Israeli wakasema, Tuambieni huo uovu ulikuwaje kutendeka?

4. Huyo Mlawi, huyo mume wa mwanamke aliyeuawa, akajibu na kusema, Mimi nilifikilia Gibea ulio wa Benyamini mimi na suria yangu, ili tulale.

5. Nao watu waume wa Gibea wakaniondokea, na kuizingira hiyo nyumba pande zote juu yangu wakati wa usiku; walidhani kuniua, na suria wangu wakamtenza nguvu, hata amekufa.

6. Basi nikamtwaa huyo suria yangu, na kumkata vipande, na kumpeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli; kwa sababu wametenda maovu makuu na upumbavu katika Israeli.

7. Angalieni, ninyi wana wa Israeli nyote, sasa toeni maneno na mashauri yenu.

8. Basi watu hao wote waliinuka kama mtu mmoja, wakisema, Hatutakwenda, hata mmoja, hemani kwake, wala hatutaondoka, hata mmoja, kwenda nyumbani kwake.

Amu. 20