17. Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za BWANA bali wao hawakufanya hivyo.
18. Na wakati BWANA alipowainulia waamuzi, ndipo BWANA alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana BWANA alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua.
19. Lakini ikawa, wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine ili kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi.
20. Basi hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu;
21. mimi nami tokea sasa sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa;
22. ili kwa njia ya hayo nipate kuwajaribu Israeli, kwamba wataishika njia ya BWANA kwenda katika njia hiyo, au sivyo.
23. Basi BWANA akawaacha mataifa yale, wala hakuwafukuza kwa upesi, wala hakuwatia katika mikono ya Yoshua.