Amu. 19:20-30 Swahili Union Version (SUV)

20. Kisha huyo mzee alisema, Na iwe amani kwako; lakini na haya yaliyokupungukia na yawe juu yangu mimi lakini usilale njiani.

21. Basi akamtia ndani ya nyumba yake, akawapa punda chakula; nao wakaosha miguu, wakala na kunywa.

22. Hapo walipokuwa wakifurahisha mioyo yao, tazama, watu wa mji huo, watu mabaradhuli wakaizingira hiyo nyumba pande zote, wakagonga mlango; wakasema na huyo mwenye nyumba, huyo mzee, na kumwambia, Mlete nje mtu yule aliyefika nyumbani kwako, ili tupate kumjua.

23. Naye mtu mwenye nyumba akawatokea hapo nje, na kuwaambia, La, sivyo, ndugu zangu nawasihi msifanye uovu jinsi hii; kwa kuwa mtu huyu ameingia ndani ya nyumba yangu, msifanye upumbavu huu.

24. Tazama, binti yangu yupo hapa, ni mwanamwali, na suria wake huyo mtu; nitawaleta hapa nje sasa nanyi watwezeni, na kuwatenda hayo myaonayo kuwa ni mema; lakini mtu huyu msimtende jambo la upumbavu namna hii.

25. Lakini hao watu hawakukubali kumsikia; basi mtu huyo akamshika suria wake, na kumleta nje kwao; nao wakamjua, na kumtenda uovu usiku kucha hata asubuhi kisha kulipoanza kupambauka wakamwacha aende zake.

26. Ndipo huyo mwanamke akaja alfajiri, akaanguka chini mlangoni pa nyumba ya mtu yule alimokuwamo bwana wake, hata kulipokucha.

27. Bwana wake akaondoka asubuhi, akaifungua milango ya nyumba, akatoka nje ili aende zake, na tazama, huyo mwanamke suria yake alikuwa ameanguka pale mlangoni pa nyumba, na mikono yake ilikuwa i pale kizingitini.

28. Akamwambia, Haya ondoka, twende zetu; lakini hakuna aliyemjibu; ndipo akamwinua akamweka juu ya punda; mtu huyo akaondoka, akaenda mahali pake mwenyewe.

29. Naye alipokwisha kuingia nyumbani mwake, akatwaa kisu, kisha akamshika huyo suria yake, akampasua kiungo kwa kiungo, vipande kumi na viwili akampeleka katika mipaka yote ya Israeli.

30. Basi ikawa, wote walioliona jambo hilo wakasema, Jambo kama hili halijatendeka wala kuonekana tangu siku hiyo wana wa Israeli walipokwea kutoka katika nchi ya Misri hata leo; haya, lifikirini, fanyeni shauri, mkanene.

Amu. 19