Amu. 18:23-30 Swahili Union Version (SUV)

23. Wakawapigia kelele wana wa Dani. Nao wakageuza nyuso zao na kumwambia Mika, Una nini wewe, hata ukaja na mkutano namna hii?

24. Akasema, Ninyi mmeichukua miungu niliyoifanya, na huyo kuhani, nanyi mmekwenda zenu, nami nina nini tena? Basi imekuwaje ninyi kuniuliza, Una nini wewe?

25. Hao wana wa Dani wakamwambia, Hiyo sauti yako isisikiwe kati yetu, wasije walio na hasira wakakuangukia, nawe ukapotewa na uhai wako, pamoja na uhai wa watu wa nyumbani mwako.

26. Basi wana wa Dani wakaenda zao; naye Mika alipoona ya kuwa ni wenye nguvu kumshinda yeye, akageuka akarudi nyumbani kwake.

27. Nao wakakitwaa hicho alichokuwa amekifanya Mika, na kuhani aliyekuwa naye nao wakafikilia Laisha, kwenye watu waliokuwa wenye starehe na hifadhi, wakawapiga kwa makali ya upanga; wakaupiga moto mji wao.

28. Wala hakuwako mwokozi, kwa sababu huo mji ulikuwa ni mbali sana na Sidoni, nao hawakuwa na shughuli na mtu awaye yote; na mji huo ulikuwa katika hilo bonde lililo karibu na Bethrehobu. Nao wakaujenga huo mji na kukaa humo.

29. Wakauita mji jina lake Dani, kwa kuliandama jina la baba yao Dani, aliyezaliwa kwake Israeli; lakini jina la mji huo hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Laisha.

30. Kisha wana wa Dani wakajisimamishia hiyo sanamu ya kuchonga; na Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, yeye na wanawe walikuwa ni makuhani katika kabila ya Wadani hata siku ya kuchukuliwa mateka hiyo nchi.

Amu. 18