Amu. 18:16-28 Swahili Union Version (SUV)

16. Hao watu mia sita wenye kuvaa silaha zao za vita, waliokuwa ni wana wa Dani, wakasimama penye maingilio ya lango.

17. Na hao watu watano waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi wakakwea juu, wakaingia ndani, na kuitwaa hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu; na huyo kuhani akasimama penye maingilio ya lango pamoja na hao watu waume sita mia wenye kuvaa silaha za vita.

18. Nao hapo walipoingia ndani ya nyumba ya Mika, na kuileta hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu, huyo kuhani akawauliza, Je! Mwafanya nini ninyi?

19. Wao wakamwambia, Nyamaza wewe, weka mkono wako kinywani mwako, uende pamoja nasi, uwe kwetu baba, tena kuhani; je! Ni vema kwako kuwa kuhani kwa ajili ya nyumba ya mtu mmoja, au kuwa kuhani kwa ajili ya kabila na jamaa katika Israeli?

20. Huyo kuhani moyo wake ukafurahi, naye akaitwaa hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kuchonga, akaenda katikati ya hao watu.

21. Basi wakageuka wakaenda zao, lakini watoto wadogo na wanyama wao wa mifugo, na vyombo vyao, wakawatanguliza mbele yao.

22. Walipokuwa wamekwenda kitambo kizima kutoka nyumba ya Mika, wale watu waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na nyumba ya Mika walikutana, wakawaandama na kuwapata hao wana wa Dani.

23. Wakawapigia kelele wana wa Dani. Nao wakageuza nyuso zao na kumwambia Mika, Una nini wewe, hata ukaja na mkutano namna hii?

24. Akasema, Ninyi mmeichukua miungu niliyoifanya, na huyo kuhani, nanyi mmekwenda zenu, nami nina nini tena? Basi imekuwaje ninyi kuniuliza, Una nini wewe?

25. Hao wana wa Dani wakamwambia, Hiyo sauti yako isisikiwe kati yetu, wasije walio na hasira wakakuangukia, nawe ukapotewa na uhai wako, pamoja na uhai wa watu wa nyumbani mwako.

26. Basi wana wa Dani wakaenda zao; naye Mika alipoona ya kuwa ni wenye nguvu kumshinda yeye, akageuka akarudi nyumbani kwake.

27. Nao wakakitwaa hicho alichokuwa amekifanya Mika, na kuhani aliyekuwa naye nao wakafikilia Laisha, kwenye watu waliokuwa wenye starehe na hifadhi, wakawapiga kwa makali ya upanga; wakaupiga moto mji wao.

28. Wala hakuwako mwokozi, kwa sababu huo mji ulikuwa ni mbali sana na Sidoni, nao hawakuwa na shughuli na mtu awaye yote; na mji huo ulikuwa katika hilo bonde lililo karibu na Bethrehobu. Nao wakaujenga huo mji na kukaa humo.

Amu. 18