Amu. 18:10-23 Swahili Union Version (SUV)

10. Hapo mtakapokwenda mtawafikilia watu wakaao salama salimini, na hiyo nchi nayo ni kubwa; kwa kuwa Mungu ameitia mikononi mwenu; ni mahali ambapo hapana kupungukiwa na kitu cho chote kilicho duniani.

11. Basi wakatoka hapo watu mia sita waliovaa silaha za vita, wa jamaa ya Wadani, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli.

12. Wakakwea juu na kupiga kambi huko Kiriath-yearimu, katika Yuda; kwa sababu hiyo wakapaita mahali pale jina lake Mahane-dani hata hivi leo; tazama, ni hapo nyuma ya Kiriath-yearimu.

13. Nao wakapita huko hata hiyo nchi ya vilima vilima ya Efraimu, wakafikilia nyumba ya huyo Mika.

14. Ndipo hao watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laisha wakajibu, na kuwaambia ndugu zao Je! Ninyi mwajua ya kwamba mna naivera ndani ya nyumba hizi, na kinyago na sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu? Basi sasa fikirini iwapasayo kufanya.

15. Basi wakageuka wakaenda kuko, wakafikilia nyumba ya huyo hirimu, Mlawi, hata hiyo nyumba ya Mika, nao wakamwuliza habari za hali yake.

16. Hao watu mia sita wenye kuvaa silaha zao za vita, waliokuwa ni wana wa Dani, wakasimama penye maingilio ya lango.

17. Na hao watu watano waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi wakakwea juu, wakaingia ndani, na kuitwaa hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu; na huyo kuhani akasimama penye maingilio ya lango pamoja na hao watu waume sita mia wenye kuvaa silaha za vita.

18. Nao hapo walipoingia ndani ya nyumba ya Mika, na kuileta hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu, huyo kuhani akawauliza, Je! Mwafanya nini ninyi?

19. Wao wakamwambia, Nyamaza wewe, weka mkono wako kinywani mwako, uende pamoja nasi, uwe kwetu baba, tena kuhani; je! Ni vema kwako kuwa kuhani kwa ajili ya nyumba ya mtu mmoja, au kuwa kuhani kwa ajili ya kabila na jamaa katika Israeli?

20. Huyo kuhani moyo wake ukafurahi, naye akaitwaa hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kuchonga, akaenda katikati ya hao watu.

21. Basi wakageuka wakaenda zao, lakini watoto wadogo na wanyama wao wa mifugo, na vyombo vyao, wakawatanguliza mbele yao.

22. Walipokuwa wamekwenda kitambo kizima kutoka nyumba ya Mika, wale watu waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na nyumba ya Mika walikutana, wakawaandama na kuwapata hao wana wa Dani.

23. Wakawapigia kelele wana wa Dani. Nao wakageuza nyuso zao na kumwambia Mika, Una nini wewe, hata ukaja na mkutano namna hii?

Amu. 18