1. Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; tena katika siku hizo kabila ya Wadani wakajitafutia urithi wapate mahali pa kukaa; maana hata siku hiyo urithi wao haujawaangukia kati ya kabila za Israeli.
2. Basi wana wa Dani wakatuma watu wa jamaa zao, watu watano katika hesabu yao yote, watu mashujaa, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli, ili kuipeleleza hiyo nchi, kuiaua; wakawaambia, Haya, endeni mkaikague nchi hii; basi wakaifikilia nchi ya vilima vilima ya Efraimu, hata nyumba ya huyo Mika, Wakalala huko.
3. Basi hapo walipokuwa karibu na nyumba ya Mika, wakatambua sauti yake huyo hirimu, huyo Mlawi; ndipo wakageuka wakaenda kuko, na kumwuliza, Je! Ni nani aliyekuleta wewe huku? Nawe wafanya nini mahali hapa? Una kazi gani hapa?
4. Naye akawaambia, Hivi na hivi ndivyo alivyonifanyia Mika, ameniajiri, nami nimekuwa kuhani wake.
5. Nao wakamwambia, Tafadhali tutakie shauri la Mungu, ili tupate kujua kwamba njia yetu tuiendeayo itafanikiwa.
6. Kuhani akawaambia, Haya endeni na amani; njia mnayoiendea i mbele za BWANA.
7. Ndipo hao watu watano wakaenda zao, wakafika Laisha, wakawaona wale watu waliokuwamo ndani yake, jinsi walivyokaa salama salimini kwa mfano wa walivyokaa hao Wasidoni, wenye starehe na hifadhi, kwa maana hapakuwa na mtu katika nchi hiyo aliyekuwa na amri, aliyeweza kuwatweza katika neno lo lote, nao walikuwa wa mbali na hao Wasidoni, wala hawakuwa na shughuli na mtu ye yote.
8. Kisha wakawarudia ndugu zao huko Sora na Eshtaoli; ndugu zao wakawauliza; Haya, mna habari gani?