Amu. 17:1-6 Swahili Union Version (SUV)

1. Wakati huo alikuwako mtu mmoja wa nchi ya vilima ya Efraimu, ambaye jina lake alikuwa akiitwa Mika.

2. Naye akamwambia mama yake, Hizo fedha elfu na mia moja ulizonyang’anywa, ambazo uliweka kiapo kwa ajili yake na kusema masikioni mwangu, tazama, ninazo mimi hizo fedha; ni mimi niliyezitwaa. Mama yake akasema, mwanangu na abarikiwe na BWANA.

3. Basi akamrudishia mama yake hizo fedha elfu na mia moja. Mama yake akasema, Mimi naziweka fedha hizi kabisa ziwe wakfu kwa BWANA, zitoke mkononi mwangu kwa ajili ya mwanangu, ili kufanya sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu; basi kwa hiyo nakurudishia wewe.

4. Basi hapo alipomrudishia mama yake hizo fedha, mama yake akatwaa fedha mia mbili, akampa fundi mwenye kusubu fedha, naye akafanya sanamu ya kuchonga kwazo, na sanamu ya kusubu; ambazo zilikuwa ndani ya nyumba ya Mika.

5. Basi mtu huyo Mika alikuwa na nyumba ya miungu, naye akafanya naivera, na kinyago, akamweka wakfu mmoja miongoni mwa wanawe, akawa kuhani wake.

6. Siku hizo hapakuwa na mfalme katika israeli; kila mtu alifanya hayo aliyoyaona kuwa ni mema machoni pake mwenyewe.

Amu. 17