Amu. 16:1-12 Swahili Union Version (SUV)

1. Samsoni akaenda Gaza, akaona huko mwanamke kahaba, akaingia kwake.

2. Watu wa Gaza wakaambiwa, ya kwamba, huyo Samsoni amekuja huku. Wakamzingira, wakamvizia usiku kucha, penye lango la mji, wakanyamaza kimya usiku kucha, wakisema, Na tungoje mpaka mapambazuko, ndipo tutamwua.

3. Basi Samsoni akalala hata usiku wa manane, akaondoka katikati ya usiku, akaishika milango ya lango la mji, na miimo yake miwili, akaing’oa pamoja na komeo lake, akajitwika mabegani, akavichukua hata kilele cha mlima ule unaokabili Hebroni.

4. Ikawa baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki, jina lake akiitwa Delila.

5. Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja.

6. Delila akamwambia Samsoni, Tafadhali uniambie asili ya nguvu zako nyingi, na jinsi uwezavyo kufungwa, ili uteswe.

7. Samsoni akamwambia, Wakinifunga kwa kamba mbichi saba ambazo hazijakauka bado, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu.

8. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamletea kamba mbichi saba zisizokauka, naye akamfunga nazo.

9. Na yule mwanamke alikuwa na watu katika chumba cha ndani, wakimwotea. Basi akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Ndipo akazikata zile kamba kama vile uzi wa pamba ukatwavyo ukiguswa na moto. Basi hiyo asili ya nguvu zake haikujulikana.

10. Delila akamwambia Samsoni, Tazama, umenidhihaki, na kuniambia uongo; sasa tafadhali, niambie, waweza kufungwa kwa kitu gani?

11. Akamwambia Wakinifunga tu kwa kamba mpya ambazo mtu hakufanya kazi nazo, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu.

12. Basi Delila akatwaa kamba mpya akamfunga nazo, akamwambia, Wafilisti wanakujia, Samsoni. Na wale wenye kuotea walikuwa katika chumba cha ndani. Naye akazikata, akazitupa kutoka mikononi mwake kama uzi.

Amu. 16