Amu. 15:2-12 Swahili Union Version (SUV)

2. Baba yake akasema, Hakika mimi nalidhani ya kuwa umemchukia kabisa; basi nalimpa rafiki yako. Je! Ndugu yake mdogo mzuri kuliko yeye? Tafadhali, mtwae huyo badala yake.

3. Samsoni akasema, Safari hii nitakuwa sina hatia katika habari za hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru.

4. Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa vienge vya moto akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia kienge kati ya kila mikia miwili.

5. Alipokwisha kuviwasha moto vile vienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni.

6. Ndipo Wafilisti wakasema, Ni nani aliyetenda hivi? Wakasema, Ni huyo Samsoni, mkwewe yule Mtimna, kwa sababu alimchukua mkewe akampa mwenzake. Wafilisti wakaenda wakamteketeza yeye na baba yake kwa moto.

7. Samsoni akawaambia, Ikiwa ninyi mnafanya mambo kama hayo, hakika nitajilipiza kisasi juu yenu, na baadaye nitakoma.

8. Akawapiga upeo, mapigo makuu sana, kisha akatelemka akakaa katika ufa wa jabali la Etamu.

9. Basi Wafilisti wakapanda wakapiga kambi yao katika Yuda, wakajieneza katika Lehi.

10. Watu wa Yuda wakasema, Mbona mmekuja kupigana nasi? Wakasema, Tumepanda ili kumfunga Samsoni, kumtenda yeye kama alivyotutenda sisi.

11. Ndipo watu elfu tatu wa Yuda wakatelemka hata ule ufa wa jabali la Etamu, wakamwambia Samsoni, Je! Hujui ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hii, basi, uliyotutenda? Akawaambia, Kadiri ile walivyonitenda mimi, ndivyo nilivyowatenda wao.

12. Wakamwambia, Tumeshuka ili kukufunga, tupate kukutia katika mikono ya Wafilisti. Samsoni akawaambia, Niapieni ya kwamba ninyi wenyewe hamtaniangukia.

Amu. 15