Amu. 13:15-24 Swahili Union Version (SUV)

15. Kisha Manoa akamwambia huyo malaika wa BWANA, Nakuomba, tukuzuie, ili tupate kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako.

16. Lakini malaika wa BWANA akamwambia Manoa, Ujapokuwa wanizuia, sitakula katika mkate wako; na kwamba wataka kufanya tayari sadaka ya kuteketezwa, inakupasa kumsongezea BWANA. Kwa kuwa Manoa hakujua ya kwamba yeye ni malaika wa BWANA.

17. Manoa akamwambia huyo malaika wa BWANA, Jina lako ni nani, ili kwamba hapo hayo maneno yako yatakapotimia nipate kukutukuza?

18. Huyo malaika wa BWANA akamwambia, Kwani wewe kuniuliza jina langu, kwa kuwa jina hilo ni la ajabu?

19. Basi Manoa akamtwaa yule mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, akamtolea BWANA hapo juu ya mwamba; huyo malaika akatenda la ajabu; Manoa na mkewe wakaangalia.

20. Kwa maana, ikawa, mara huo mwali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa BWANA akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakainama kifudifudi.

21. Lakini malaika wa BWANA hakumtokea Manoa tena, wala mkewe. Ndipo Manoa alipojua ya kwamba ndiye malaika wa BWANA.

22. Manoa akamwambia mkewe, Hakika yetu tutakufa sisi, kwa sababu tumemwona Mungu.

23. Lakini mkewe akamwambia, Kama BWANA angetaka kutuua hangepokea sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, mikononi mwetu, wala hangetuonyesha mambo hayo yote, wala hangetuambia mambo kama hayo wakati huu.

24. Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, BWANA akambarikia.

Amu. 13