Amu. 11:5-19 Swahili Union Version (SUV)

5. Ikatukia, hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu;

6. wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni.

7. Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Basi kwani kunijilia hivi sasa wakati mlio katika taabu?

8. Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Kwa ajili ya hayo sasa tumegeuka kukuelekea wewe tena, ili uende pamoja nasi na kupigana na wana wa Amoni, nawe utakuwa kichwa chetu juu ya wenyeji wote wa Gileadi.

9. Basi Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi Kwamba mwanirejeza kwetu tena ili kupigana na wana wa Amoni, naye BWANA akiwatoa mbele yangu, je! Mimi nitakuwa kichwa chenu?

10. Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Yeye BWANA atakuwa shahidi kati yetu; hakika yetu tutafanya sawasawa na neno lako.

11. Ndipo Yeftha akaenda pamoja na wazee wa Gileadi, na hao watu wakamfanya awe kichwa, tena mkuu, juu yao; naye Yeftha akanena maneno yake yote mbele ya BWANA huko Mispa.

12. Basi Yeftha akatuma wajumbe waende kwa mfalme wa wana wa Amoni akasema, Je! Wewe una nini nami, hata umenijilia kupigana juu ya nchi yangu?

13. Mfalme wa wana wa Amoni akawajibu hao wajumbe wa Yeftha Kwa sababu Israeli waliitwaa nchi yangu, hapo walipokwea kutoka katika nchi ya Misri, tokea Arnoni mpaka Yaboki, na hata Yordani; basi sasa rudisha hizo nchi tena pasipo matata.

14. Yeftha akatuma wajumbe mara ya pili waende kwa huyo mfalme wa wana wa Amoni;

15. akamwambia, Yeftha akuambia hivi; Israeli hakuitwaa nchi ya Moabu, wala nchi ya wana wa Amoni;

16. lakini hapo walipokwea kutoka Misri, na Israeli walienenda katika bara hata kuifikilia Bahari ya Shamu, na kufikilia Kadeshi;

17. ndipo Israeli wakatuma wajumbe waende kwa mfalme wa Edomu, wakisema, Nakuomba sana unipe ruhusa nipite katika nchi yako; lakini mfalme wa Edomu hakusikia. Ni vivyo wakampelekea wajumbe mfalme wa Moabu; wala yeye hakukubali; basi Israeli wakakaa katika Kadeshi.

18. Kisha akaenda nyikani na kuizunguka hiyo nchi ya Edomu, na nchi ya Moabu, nao wakapita upande wa mashariki wa nchi ya Moabu, wakapanga marago upande wa pili wa Arnoni; wala hawakuingia ndani ya mpaka wa Moabu, kwa maana Arnoni ilikuwa ni mpaka wa Moabu.

19. Kisha Israeli wakatuma wajumbe waende kwa Sihoni mfalme wa Waamori, mfalme wa Heshboni: Israeli wakamwambia, Twakuomba utupe ruhusa tupite katika nchi yako, mpaka mahali pangu.

Amu. 11