Amu. 1:1-19 Swahili Union Version (SUV)

1. Ikawa baada ya kufa kwake Yoshua, wana wa Israeli wakamwuliza BWANA, wakisema, Ni nani atakayekwea kwanza kwa ajili yetu juu ya Wakanaani, ili kupigana nao?

2. BWANA akasema, Yuda atakwea; tazama, nimeitia hiyo nchi mkononi mwake.

3. Ndipo Yuda akamwambia Simeoni ndugu yake, Kwea wewe pamoja nami katika kura yangu, ili tupate kupigana na Wakanaani; kisha mimi nami nitakwenda pamoja nawe katika kura yako. Basi Simeoni akaenda pamoja naye.

4. Yuda akakwea; naye BWANA akawatia Wakanaani na Waperizi mkononi mwao; nao wakawapiga huko Bezeki watu elfu kumi.

5. Wakampata huyo Adoni-bezeki huko Bezeki; wakapigana naye, nao wakawapiga Wakanaani na Waperizi.

6. Lakini Adoni-bezeki akakimbia; nao wakamwandamia na kumshika, wakamkata vyanda vyake vya gumba vya mikono na vya miguu.

7. Adoni-bezeki akasema, Wafalme sabini, waliokuwa wamekatwa vyanda vyao vya gumba vya mikono na vya miguu, waliokota chakula chao chini ya meza yangu; kama nilivyofanya mimi, Mungu amenilipa vivyo. Wakamleta Yerusalemu naye akafa kuko.

8. Kisha wana wa Yuda wakapigana na Yerusalemu, wakautwaa, wakaupiga kwa makali ya upanga, na kuupiga moto huo mji.

9. Baadaye wana wa Yuda wakatelemka ili wapigane na hao Wakanaani waliokaa katika nchi ya milimani, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela.

10. Kisha Yuda akawafuatia hao Wakanaani waliokaa katika Hebroni; (jina la Hebroni hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-arba;) nao wakamwua Sheshai, na Ahimani, na Talmai.

11. Kisha kutoka hapo akawafuatia wale wenye kukaa Debiri. (Jina la Debiri hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-seferi.)

12. Huyo Kalebu alisema, Yeye atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, nitamwoza mwanangu Aksa awe mkewe.

13. Naye Othnieli, mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, aliutwaa; basi akamwoza mwanawe Aksa.

14. Ikawa hapo alipokwenda kukaa naye, huyo mwanamke akamtaka ili aombe shamba kwa baba yake; na huyo mwanamke akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Una haja gani utakayo?

15. Mwanamke akasema, Nipe baraka; kwa kuwa wewe umeniweka katika nchi ya Negebu, basi unipe na vijito vya maji pia. Kalebu akampa vile vijito vya maji vya juu na vijito vya chini.

16. Hao wana wa Mkeni, huyo shemeji yake Musa, wakakwea juu kutoka katika huo mji wa mitende, pamoja na wana wa Yuda, na kuingia hiyo nyika ya Yuda, iliyo upande wa kusini wa Aradi; nao wakaenda na kukaa pamoja na watu hao.

17. Kisha Yuda akaenda pamoja na nduguye Simeoni, na wakawapiga Wakanaani waliokaa katika Sefathi, na kuuharibu mji kabisa. Na jina la mji huo ulikuwa ukiitwa Horma.

18. Pamoja na haya Yuda aliutwaa Gaza pamoja na mipaka yake, na Ashkeloni na mipaka yake, na Ekroni na mipaka yake.

19. BWANA alikuwa pamoja na Yuda; naye akawafukuza watu waliokaa katika nchi ya milimani; asiweze kuwafukuza hao waliokaa katika hilo bonde, kwa kuwa wao walikuwa na magari ya chuma.

Amu. 1