12. Maana mimi najua jinsi maasi yenu yalivyo mengi, na jinsi dhambi zenu zilivyo kubwa; ninyi mnaowaonea wenye haki, mnaopokea rushwa, na kuwageuza wahitaji langoni wasipate haki yao.
13. Kwa ajili ya hayo mwenye busara atanyamaza kimya wakati kama huo; kwa kuwa ni wakati mbaya.
14. Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi; hivyo BWANA, Mungu wa majeshi, atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo.
15. Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba BWANA, Mungu wa majeshi, atawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu.
16. Kwa ajili ya hayo, asema BWANA, Mungu wa majeshi, aliye Bwana; Kutakuwako maombolezo katika njia kuu zote; nao watasema katika njia zote, Ole! Ole! Nao watamwita mkulima aje kuombolea, na hao walio hodari wa kulia waje kuomboleza.
17. Tena katika mashamba yote ya mizabibu kutakuwako kulia; kwa maana mimi nitapita katikati yako, asema BWANA.
18. Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya BWANA; kwani kuitamani siku ya BWANA? Ni giza, wala si nuru.
19. Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma.
20. Je! Siku ya BWANA haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga.