10. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.
11. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana,Kama tukifa pamoja naye,tutaishi pamoja naye pia;
12. Kama tukistahimili,tutamiliki pamoja naye;Kama tukimkana yeye,yeye naye atatukana sisi;
13. Kama sisi hatuamini,yeye hudumu wa kuaminiwa.Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.
14. Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao.
15. Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.
16. Jiepushe na maneno yasiyo na maana, ambayo si ya dini; kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu,
17. na neno lao litaenea kama donda-ndugu. Miongoni mwa hao wamo Himenayo na Fileto,
18. walioikosa ile kweli, wakisema ya kwamba kiyama imekwisha kuwapo, hata kuipindua imani ya watu kadha wa kadha.
19. Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii,Bwana awajua walio wake.Na tena,Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu.
20. Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina.