5. Na Washami wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akawapiga wa Washami watu ishirini na mbili elfu.
6. Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski, na hao Washami wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda.
7. Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumwa wa Hadadezeri, akazileta Yerusalemu.
8. Tena toka Tebhathi na toka Berothai, miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi mno.
9. Na Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia ya kwamba Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri,
10. Tou akamtuma kwa Daudi Hadoramu mwanawe kusalimia, na kumbarikia, kwa sababu amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou. Na mkononi mwake akaleta vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na vyombo vya shaba;
11. hivi pia mfalme Daudi akavifanya wakfu kwa BWANA, pamoja na hiyo fedha, na dhahabu alizofanya wakfu za mataifa yote aliowashinda;
12. za Edomu, na za Moabu, na za wana wa Amoni, na za Wafilisti, na za Amaleki, na za nyara za Hadadezeri, mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba.
13. Basi Daudi akajipatia jina, aliporudi kutoka kuwapiga Waedomi katika Bonde la Chumvi, watu kumi na nane elfu.