2 Sam. 22:4-18 Swahili Union Version (SUV)

4. Nitamwita BWANA astahiliye kusifiwa;Hivyo nitaokoka na adui zangu.

5. Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka,Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.

6. Kamba za kuzimu zilinizunguka;Mitego ya mauti ikanikabili.

7. Katika shida yangu nalimwita BWANA,Naam, nikamlalamikia Mungu wangu;Naye akaisikia sauti yangu hekaluni mwake,Kilio changu kikaingia masikioni mwake.

8. Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka,Misingi ya mbinguni ikasuka-sukaNa kutikisika, kwa sababu alikuwa na ghadhabu.

9. Kukapanda moshi kutoka puani mwake,Moto ukatoka kinywani mwake ukala;Makaa yakawashwa nao.

10. Aliziinamisha mbingu akashuka;Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake.

11. Akapanda juu ya kerubi akaruka;Naam, alionekana juu ya mabawa ya upepo.

12. Akafanya giza hema zake za kumzunguka,Makusanyiko ya maji, mawingu makuu ya mbinguni.

13. Toka mwangaza uliokuwa mbele zakeMakaa ya moto yakawashwa.

14. BWANA alipiga radi toka mbinguni,Naye Aliye juu akaitoa sauti yake.

15. Akapiga mishale, akawatawanya;Umeme, naye akawatapanya.

16. Ndipo ilipoonekana mikondo ya bahari,Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa,Kwa kukemea kwake BWANA,Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwake.

17. Alipeleka kutoka juu, akanishika;Akanitoa katika maji mengi;

18. Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu,Na wale walionichukia;Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi.

2 Sam. 22