32. Naye huyo Barzilai alikuwa mzee sana, amepata umri wa miaka themanini; naye amemlisha mfalme hapo alipokuwapo Mahanaimu; kwa kuwa alikuwa mtu mwenye cheo kikubwa.
33. Naye mfalme akamwambia Barzilai, Uvuke pamoja nami; nami nitakulisha kwangu huko Yerusalemu.
34. Lakini Barzilai akamjibu mfalme, Siku ni ngapi za miaka ya maisha yangu, hata mimi nipande pamoja na mfalme kwenda Yerusalemu?
35. Nimepata leo miaka themanini; nami je! Naweza kupambanua mema na mabaya? Mimi mtumwa wako, je! Naweza kuonja nilacho au ninywacho? Naweza kusikia tena sauti ya waimbaji waume na wake? Kwa nini basi mtumwa wako amlemee bado bwana wangu mfalme?
36. Mtumwa wako ataka kuvuka Yordani tu pamoja na mfalme; tena mbona mfalme anilipie thawabu ya namna hii?
37. Niache nirudi basi, mimi mtumwa wako, ili nife katika mji wangu mwenyewe, karibu na kaburi la baba yangu na la mama yangu. Lakini tazama, mtumwa wako Kimhamu; na avuke yeye pamoja na bwana wangu mfalme; nawe ukamtendee yeye yaliyo mema machoni pako.
38. Mfalme akajibu, Haya, Kimhamu na avuke pamoja nami, nami nitamtendea yaliyo mema machoni pako wewe; na kila utakalotaka kwangu, mimi nitalifanya kwa ajili yako.
39. Basi watu wote wakavuka Yordani, naye mfalme akavuka; kisha mfalme akambusu Barzilai, akambariki; naye akarejea mahali pake.
40. Hivyo mfalme akavuka, akafika Gilgali; Kimhamu akavuka pamoja naye; na watu wote wa Yuda wakamvusha mfalme, na nusu ya watu wa Israeli.
41. Tena, angalia, watu wote wa Israeli wakamjia mfalme wakamwambia mfalme, Kwa nini ndugu zetu, watu wa Yuda wamekuiba, na kumvusha Yordani mfalme, na jamaa yake, na watu wote wa Daudi pamoja naye?
42. Ndipo watu wote wa Yuda wakawajibu hao watu wa Israeli, Ni kwa sababu mfalme ndiye wa jamaa yetu; mbona basi ninyi mmekasirika kwa ajili ya jambo hili? Je! Sisi tumekula kitu cha mfalme? Ama ametupa sisi zawadi yo yote?
43. Hao watu wa Israeli wakawajibu watu wa Yuda, wakasema, Sisi tunazo sehemu kumi katika mfalme, tena tunayo haki yetu katika Daudi zaidi kuliko ninyi; mbona basi ninyi mmetudharau sisi, lisitakwe kwanza shauri letu katika kumrudisha tena mfalme wetu? Na maneno ya watu wa Yuda yakawa makali kuliko maneno ya watu wa Israeli.