25. Naye mfalme akamwambia Sadoki, Rudisha sanduku la Mungu mjini; nikipata kibali machoni pa BWANA atanirudisha, na kunionyesha tena sanduku hili, na maskani yake;
26. lakini akisema kama hivi, Mimi si radhi nawe kabisa; basi, mimi hapa, na anitendee kama aonavyo kuwa vyema.
27. Kisha mfalme akamwambia Sadoki, kuhani, Angalia, rudini mjini kwa amani, na wana wenu wawili pamoja nanyi, Ahimaasi, mwana wako, na Yonathani, mwana wa Abiathari.
28. Angalia, mimi nitangoja penye vivuko vya jangwani, hata litakaponifikilia neno la kunipasha habari kutoka kwenu.
29. Basi Sadoki na Abiathari wakalichukua sanduku la Mungu, wakalirudisha Yerusalemu; wakakaa huko.
30. Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda.