12. Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao;
13. Wakipatikana na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa; wamekuwa ni mawaa na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi;
14. wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana;
15. wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu;
16. lakini alikaripiwa kwa uhalifu wake mwenyewe; punda, asiyeweza kusema, akinena kwa sauti ya kibinadamu, aliuzuia wazimu wa nabii yule.
17. Hawa ni visima visivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani, ambao weusi wa giza ni akiba waliyowekewa.
18. Maana wakinena maneno makuu mno ya kiburi, kwa tamaa za mwili na kwa ufisadi huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu;
19. wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule.
20. Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.
21. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa.
22. Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni.